Mlipuko huo ulitokea karibu na msikiti katika mji wa Mastung siku ya Ijumaa wakati watu walipokuwa wakikusanyika kusherehekea Maulidi yaani kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW). Hayo yamedokezwa na kamishna msaidizi wa eneo hilo Attahul Munim.
Taarifa zinasema naibu msimamizi wa polisi wa Mastung (DSP) Nawaz Gashkori, ambaye alikuwepo kwenye mkutano huo, pia aliuawa.
Maafisa wa usalama wamedokeza kuwa gaidi aliyetekeelza hujuma ya kwanza alijilipua karibu na gari la DSP.
Idadi ya vifo inatarajiwa kuongezeka kwani baadhi ya waliojeruhiwa wako katika hali mbaya.
Saa chache baada ya mlipuko huo katika jimbo la Balochistan, mlipuko mwingine ulikumba msikiti mmoja katika mkoa wa Khyber Pakhtunkhwa ambao pia unapakana na Afghanistan, na kuua watu wasiopungua wawili.
Paa la msikiti huo liliporomoka katika mlipuko huo, na kuacha takriban watu 30 hadi 40 wamenasa chini ya vifusi.
Maafisa wa Pakistan walilaani mashambulizi hayo, wakilaumu hatua hiyo kwa maadui wanaotaka kuzusha mifarakano katika eneo hilo.
Waziri wa habari wa muda wa Balochistan Jan Achakzai alisema "Adui anataka kuharibu uvumilivu wa kidini na amani katika Balochistan". Huku akisema magaidi waliotekeleza hujuma hiyo wanapata himaya ya kigeni, amesisitiza kuwa ugaidi huo hauwezi kuvumiliwa."Achakzai alisema Waziri Kiongozi wa Balochistan anayeshikkilia nafasi hiyo kwa muda, Ali Mardan Domki, ameagiza vikosi vya usalama kuwakamata waliohusika na mlipuko huo. Bado hakuna kundi ambalo limedai kuhusika na shambulio hilo.
Waziri wa mambo ya ndani wa Pakistan, Sarfraz Ahmed Bugti, pia alilaani mlipuko huo, akisema kuwa "magaidi hawana dini."
Wakati huo huo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vitendo vya ugaidi huku ikitoa salamu za rambirambi kwa serikali na wananchi wa Pakistani hususan manusura wa wahanga na kuwaombea ahueni ya haraka majeruhi hao.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Nasser Kana’ani alisema mashambulizi hayo ni "mfano wa wazi wa magaidi kujitenga na mafundisho ya rehema ya Mtume Muhammad (SAW)".